TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA
HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa Umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue
fever” hapa nchini.Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa
kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es Salaam kupelekwa
kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya
homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya
wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu ni 400 na Vifo 3. Kwa wiki
iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar es
salaam ni 60 (42-Kinondoni, 14-Temeke na 4-Ilala) na idadi ya wagonjwa waliopo
wodini mpaka sasa ni 13.
Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini
kwani uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo
idadi ya watu 40 walithibitika kuwa na ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi
Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuugua ugonjwa huu.
Homa ya
Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na
kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dengue ni ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi
za ukanda wa joto. Takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika
nchi zenye ugonjwa huu. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa
takribani matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka. Watu laki
5 hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya Dengue imeshatokea
katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.
