Showing posts with label DENGUE DEATHS. Show all posts
Showing posts with label DENGUE DEATHS. Show all posts

Wednesday, May 14, 2014

HOMA YA DENGUE: TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa Umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa nchini.Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es Salaam kupelekwa kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu ni 400 na Vifo 3. Kwa wiki iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar es salaam ni 60 (42-Kinondoni, 14-Temeke na 4-Ilala) na idadi ya wagonjwa waliopo wodini mpaka sasa ni 13.

Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu 40 walithibitika kuwa na ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuugua ugonjwa huu.

Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dengue ni ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi za ukanda wa joto. Takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi zenye ugonjwa huu. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa takribani matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka. Watu laki 5 hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya Dengue imeshatokea katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.