TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA
HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa Umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue
fever” hapa nchini.Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa
kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es Salaam kupelekwa
kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya
homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya
wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu ni 400 na Vifo 3. Kwa wiki
iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar es
salaam ni 60 (42-Kinondoni, 14-Temeke na 4-Ilala) na idadi ya wagonjwa waliopo
wodini mpaka sasa ni 13.
Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini
kwani uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo
idadi ya watu 40 walithibitika kuwa na ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi
Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuugua ugonjwa huu.
Homa ya
Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na
kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dengue ni ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi
za ukanda wa joto. Takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika
nchi zenye ugonjwa huu. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa
takribani matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka. Watu laki
5 hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya Dengue imeshatokea
katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.
Hapa Afrika Dengue ni ugonjwa unaojulikana kwa
kiwango kidogo sana. Licha ya kwamba milipuko ya kwanza imetokea tangu mwanzoni
wa karne ya 19. Matukio ya Ugonjwa huu yameongezeka Afrika tangu miaka ya 1980,
matukio mengi yakitokea nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ikiwa ni pamoja
na Msumbiji, Somalia, Kenya, Komoro, Djibouti na Tanzania. Ikumbukwe kuwa jina
“Dengue” linatokana na neno “Dinga” la kiswahili linalolomaanisha ugonjwa
unaotakana na pepo yaani Kudinga pepo. Mabaharia wa Kispanish walipokuja kwenye
pwani ya Afrika Mashariki walirudi kwao na kuuita “Dengue”.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza
kujitokeza kuanzia katisiku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa
ya dengue. Kwa wakati mwingine dalili za
ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi
wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana
vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kuna aina 3 tofauti za namna ugonjwa huu
unavyoweza kujitokeza iwapo mtu aking`atwa na mbu mwenye virusi hivi;
i.Homa ya dengue (Dengue Febrile Illness): Aina hii huambatanana
dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au
uchovu.Aidha, kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa
wamejitokeza na dalili hizi.
ii.Dengue ya damu (Dengue Haemorrhagic
Fever): Aina hii yahoma ya dengue huambatana na dalili za mgonjwa kutokwa
na damu kwenye fizi au puani, vile vile kutokwa na damu chini ya ngozi.Iwapo
mgonjwa huyu ataumia sehemu yoyote ni rahisi kwake kupoteza damu nyingi kupitia
kwenye michubuko.
iii.Dengue ya kupoteza fahamu (Dengue
Shock syndrome): Aina hii ya homa ya dengue huambatana na mgonjwa kupoteza damu
nyingi ambayo hupelekea mgonjwakupoteza fahamu. Dalili hizi zimeonekana kwa
mgonjwa 1 kati ya wagonjwa 400 waliokwisha kuthibitishwa kuwa na ugonjwa hapa
nchini.
Kirusi cha homa ya Dengue kinaambukizwa kutoka
mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa Jamii ya Aedes, na hasa Aedes
aegypti. Mbu huyu anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu. Huuma wakati
ya mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani majira ya
asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa
kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari,
ndoo, vikopo, na kadhalika. Kwa bahati mbaya mbu huyu huweza kuzaliana katika
vifaa vidogo vidogo ambavyo watu wengi huvidharau. Hivi ni pamoja na makopo ya
kuotesha maua, vikombe, vifuu vya nazi, na kadhalika. Majani mapana
yanayohifadhi maji ni mazingira mazuri kwa kuzaliana kwa mbu huyu, hivyo maeneo
ya bustani siyo ajabu kuwa mahali pazuri kwa mbu hawa.
Ugonjwa huu hauambukizi kwa kumhudumia mgonjwa au
kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Homa ya dengue inaweza kutibika kama
mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna dawa maalumu ya ugonjwa wala chanjo
bali mgonjwa anatibiwa kutokana nadalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama
vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa
matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya
dengue Kuangamiza
mazalio ya mbu
·
Fukia madimbwi ya maji yaliyotuamaau nyunyuzia viuatilifu vya kuua
viluwiluwivya mbu kwenye madimbwi hayo
·
Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile:
vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
·
Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
·
Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji
kutuama
·
Funika mashimo ya maji takakwa mfuniko imara
·
Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
Kujikinga na kuumwa na mbu
·
Tumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”
·
Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
·
Tumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala
majira ya mchana na hasa kwa watoto)
·
Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zilizochukuliwa na Wizara
(i)Hatua za Dharura
Uratibu
·
Timu ya Taifa ya Maafa inayoshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wa
Halmashauri za Jiji na Wadau wa Maendeleo hukutana kila mara 2 kwa wiki
kutathmini mikakati ya dharura iliyowekwa.
Uelemishaji
na Uhamasishaji wa Jamii
·
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa tamko la Serikali kwa
nyakati tofauti kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Dengue. Tamko la kwanza lilitolewa
kwenye vyombo vya habari tarehe 04 Februari 2014 na Machi 2014.
·
Kuendelea kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa
Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara. Aidha taarifa hii pia
iinajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Ukweli
Kuhusu Ugonjwa“(Fact sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya
kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya
ugonjwa huu vitatolewa.
·
Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio, na Runinga.
Aidha Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za jiji wameendelea kutumia
Maafisa Afyaikiwemo wa kata kuwaelemisha wananchi namna ya kudhibiti ugonjwa
kwakutumia vipaza sauti, uongozi wa mitaa
Mafunzo kwa Watalaam wa Afya
·
Kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa Watumishi wa Afya ikiwa pamoja
na madaktari na mafundi maabara namna ya kutambua ugonjwa huu. Aidha watumishi
wa hospitali za Muhimbili, Mwananyamala, Amana na Temeke wamekwisha kupewa
mafunzo haya na bado wanaendelea kupewa kupitia mikutano yao ya asubuhi
(Clinical meetings). Mafunzo haya pia yanaendelea kutolewa kwa vituo vya chini
kupitia Halmashauri
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na
mawasiliano
·
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea
huduma za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa saveilensi ya Wizara. Aidha,
pamoja na Mwongozo huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa maelekezo kwa
Waganga wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini kutoa taarifa za wagonjwa wa
Dengue Fever kupitia taarifa za kila juma.
·
Kutoa miongozo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika maeneo ya
mipakani kuhusu kutokuwepo kwa aina yoyote ya vikwazo vitakavyowekwa kwa ajili
kwa wasafiri. Aidha maelekezo hayo yameainisha kuwa iwapo msafiri anayeondoka
au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa
mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa
·
Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyo kuwa
ya malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina
iwapo kuna ugonjwa huu. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeshafanya utafiti
mkoani Kagera, Morogoro na Kigoma na kuthibitisha kuwa haijaadhirika na dengue.
·
Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika
Hospitali za Manispaa za jiji la Dar es Salaam (Mwananyamala, Amana na Temeke).
Aidha, Kituo cha ‘International School of Tanganyika – IST’ kilichopo Manispaa
ya Kinondoni na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaendelea na ufuatiliaji wa
ugonjwa huu. Aidha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itafungua pia vituo mkoani
Tanga na Mtwara, mikoa imayopakana na nchi jirani yaani Kenya na Msumbiji
ambako ugonjwa huu pia umetolewa taarifa.
·
·Kupeleka taarifa ya mlipuko huu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)
kama mwongozo wa Kanuni za Afya za Kimataifa uvyaoelekeza.
Upimaji na Tiba
·
Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara
ya Taifa (NHLQATC) iliyopo NIMR. Vile vile Wizara imepeleka vipimo sawia yaani
“Dengue Rapid Test Kits” kwa vituo vya Dar es Salaam kuimarisha utambuzi. Vituo
hivo ni pamoja na hospitali za Muhimbili, Amana, Mwananyamala, Temeke Hospital,
na IST kliniki. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeagiza Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) kuhakikisha vitendanishi hivi vinakuwepo ili kurahisisha upatikanaji wake
kwa Halmashauri zote na kupelekwa kwenye vituo vya chini zaidi. Wizara imeagiza
vipimo sawia 750 vya kunyongeza ambavyo tunatarajiwa kuvipata tarehe 22.5.2014
·
Wizara imeweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa Tiba vinapatikana
wakati wote katika vituo vyote kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa
watakaogundulika na kuwa na ugonjwa huu.
Udhibiti wa mbu na mazalia
·
Kudhibiti mbu kupitia kwa kupulizia na kunyunyizia viuatilifu
katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika katika mkoa wa Dar es salaam ambayo
wametoka wagonjwa wengi wa Dengue. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu na
viluwiluwi.
Utafiti
Taasisi ya Utafiti ya magonjwa ya Binadamu (NIMR)
iko katika maandalizi ya kufanya utafiti kuhusu dengue kwa kuangalia maaeneo
makubwa mawili.
·
Ukubwa
wa tatizo katika binadamu
·
Mbu waambukizao ugonjwa wa homa ya Dengue- kujua jamii husuka,
tabia ya kuuma watu, wapi wanapopendelea kuuma, wapi wanakozaliana kwa wingi na
mazingira yao ya kawaida.
Tafiti hizi zinaanzia Dar es Salaam na kuhusisha
wilaya zote tatu (Ilala, Kinondoni, Temeke). Tafiti zitaendelea katika baadhi
ya mikoa, ikiwa ni pamoja na mikoa 8 ambako vituo vyetu vipo.Takwimu zitakazopatikana
zitaboresha mbinu za kupambana na ugonjwa huu
(ii)Hatua za Kudumu
·
WAUJ imeandaa Mpango wa wa namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Homa
ya Dengue. Mpango huu kwa kushirikisha sekta mbalimbali.
·
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa Dengue
Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu
ugonjwa huu kwani hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa majimaji
yanayotoka kwa mgonjwa. Hata hivyo tunawashauri wananchi kwenda kwenye vituo
vya afya haraka pindi wanonapo dalili za ugonjwa huu.
Mlipuko wa Dengue unadhihirisha kuwa mazingira
yetu tunayoishi si salama. Ikumbukwe kuwa, kwa sehemu kubwa, ugonjwa huu
unachochewa na mazingira machafu. Aidha mvua hizi kubwa zinazoendelea
zonachangia kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka
katika miji yetu hauridhishi kiasi ambacho kinatoa fursa kwa mazalio ya mbu
kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya binadamu.
Kwa kuwa, hadi sasa hakuna chanjo wala dawa
maalumu kwa ajili ya kudhibiti au kutibu ugonjwa huu, njia kubwa ya kupambana na ugonjwa huu ni kumzuia binadamu asimwe na
mbu. Hivyo basi, mbinu shirikishi za kutokomeza mbu inabidi zitiliwe mkazo
katika mapambano dhidi ya homa ya Dengue. Njia bora na rahisi ni kuhakikisha
mazalio yote ya mbu yanatokomezwa. Na hili laweza kufanywa na kila mtu kwa
nafasi yake.Tunashauri watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu na dawa
zinazofukuza mbu (mosquito repellent). Tunaelewa kuwa si kila mtu atakuwa na
uwezo wa kununua dawa hizi na ndiyo maana tunakazania swala la kuangamiza
mazalia ya mbu ambalo ni jukumu letu wote.Tunaendelea kuhamisisha watu na hasa
watoto walale ndani ya vyandarua venye viatilifu wanapolala wakati wa mchana.
Ningependa kuwakumbusha wananchi wa Tanzania
kuwa, huu ni muda muafaka wa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira yetu.
Tukitunza mazingira yetu, nayo yatatutunza na kutuepusha na maradhi
yanayoambatana na mazingira machafu.
Charles A. Pallangyo
Katibu Mkuu
12 Mei 2014
No comments:
Post a Comment