Thursday, April 17, 2014

HII NDIYO HASARA YA KUWA BAHILI BILA KUFIKIRIA:Benki iliyoporwa fedha


Juzi, majambazi wenye silaha walipora fedha zinazokisiwa kufikia Sh milioni 300 katika Benki ya Barclay's tawi la Kinondoni 'TX Market' jijini Dar es Salaam.

Mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa uporaji huo ulifanyika saa nne za asubuhi, ambapo mtu mmoja aliingia eneo la benki hiyo akiwa na gari aina ya Cresta na kuwashusha watu wawili waliokuwa wamebeba begi linalodaiwa kuwa fedha na kuingia ndani.

Mlinzi wa tawi hilo wa Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate alifuata gari hilo na kuliekeza mahali sahihi pakuegesha magari, kwani pale lilikuwa linazuia magari mengine kuingia benki. Wakati mlinzi huyo akilielekeza gari hilo mahali sahihi pa kuliegesha, watu watatu walikuja na pikipiki wakiwa wamepakizana mshikaki, ambapo wawili walishuka wakaingia ndani huku mmoja akibaki nje na pikipiki hiyo ambayo haikuzimwa.

Inadaiwa watu hao wawili wakiwa ndani ya benki hiyo, waliwaweka chini ya ulinzi wateja pamoja na wafanyakazi wote wa benki hiyo. Baada ya muda, mashuhuda hao walidai kuwa walimwona mlinzi aliyekuwa akielekeza gari mahali pa kuegesha, akipiga kelele na kukimbia huku na huko kuomba msaada. Wakati akifanya hivyo, inadaiwa wale watu wawili walitoka kwenye wakiwa na mfuko mkubwa unaodhaniwa kuwa na fedha na kupanda pikipiki waliyokuja nayo na kuondoka kwa kasi bila kukamatwa.

Watu walijitokeza kuitika wito wa kutoa msaada, huku taarifa zikitolewa kwa askari Polisi ambao walifika muda mfupi baadaye katika eneo la tukio na kufunga kamba eneo lote la benki na kuzuia watu kuingia katika eneo hilo wakati wakifanya uchunguzi wa awali.

Hata hivyo, haijajulikana kama walioingia awali na begi ndio waliokuwa na fedha zilizoporwa na wezi walitoka na begi, hivyo haijajulikana kama fedha hizo zilikuwa mikononi mwa wateja au benki, kwa kuwa hakuna askari Polisi wala mfanyakazi yeyote wa benki hiyo aliyekuwa tayari kuzungumzia tukio hilo. 

Taarifa nyingine zilizopatikana eneo benki hiyo, zilieleza kuwa nyuma ya tawi hilo kulikuwa na askari Polisi lakini sasa hawapo baada ya huduma hiyo kusisitishwa na benki hiyo ambayo iliamua kutumia walinzi wa kampuni binafsi, ambao hawakuwa na bunduki na badala yake walikuwa wanalinda kwa marungu.

Baadhi ya watu waliokuwepo eneo la tukio walilaumu taasisi za kifedha: "Inashangaza sana taasisi za kifedha badala ya kuwatumia askari Polisi kwa ulinzi wa benki zao wenyewe, wameng'ang'ania kulinda kwa kutumia walinzi wa kampuni binafsi ambao hawana hata silaha, " alisema Juma Seleman ambaye ni mfanyabiashara katika eneo hilo. Baadhi ya wananchi walilipongeza Polisi Kanda Maalum Kinondoni kwa kuwahi kufika haraka eneo la tukio na kufika na vifaa tofauti na huko nyuma ambako walikuwa wakichelewa kufika kila walipoitwa katika tukio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alikiri kutokea kwa uporaji huo, ambapo alisema watuhumiwa hao walifika eneo hilo wakiwa na risasi za moto: "Katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa, kiasi cha fedha hakijajulikana lakini ni kiasi kikubwa cha fedha. Wakimaliza kufanya tathmini itajulikana ni kiasi gani," alisema Kamanda Wambura.

SOURCE: Habari Leo

No comments: