Monday, May 12, 2014

"Vocha za Ruzuku ya Pembejeo" za futwa na Serikali

Serikali imetangaza rasmi kuondoa utaratibu wa ruzuku kwa kutumia vocha za pembejeo.

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alisema hayo jana katika hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa mwaka 2014/2015.
Alisema pamoja na mafanikio ya mpango wa ruzuku kumekuwepo na changamoto katika ngazi mbalimbali ikiwemo ubadhirifu, upotevu wa vocha na ucheleweshaji wa vocha hali inayopelekea wakulima kutopata pembejeo mapema.
“Serikali imeondoa utaratibu wa ruzuku kwa kutumia vocha,” alisema Chiza.

Kutokana na changamoto hizo Serikali kuanzia msimu wa 2013/2014 ilibuni utaratibu wa kutoa pembejeo za mbolea, mbegu za mahindi na mpunga kwa vikundi vya wakulima na vyama vya ushirika kwa kutumia mikopo kupitia taasisi za fedha.
Hata hivyo alisema utaratibu huo haukuweza kuendelea kutekelezwa kutokana na taasisi za fedha kuweka sharti kwa serikali kuweka fedha taslimu kwa dhamana kabla ya kutoa mikopo hiyo, jambo ambalo halikuwezekana.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku za pembejeo za mbegu bora na mbolea kwa wakulima kwa utaratibu wa vocha:
  • Mwaka 2008/2009 kaya 737,000 
  • Mwaka 2009/2010 kaya milioni 1.5 
  • Mwaka 2010/2011 kaya milioni 2.01
  • Mwaka 2011/2012 kaya milioni 1.7 
  • Mwaka 2012/2013 kaya 940,783 
  • Mwaka 2013/2014 kaya 932,100 
Zilitumia tani 124,685 za mbolea na tani 9621 za mbegu.



Alisema uzalishaji wa mahindi uliongezeka kutoka magunia matano hadi kufikia magunia 15 kwa ekari na uzalishaji wa mpunga uliongezeka kutoka gunia nne hadi kufikia gunia 20 kwa ekari.



Alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na taasisi za fedha zilizo tayari kutekeleza utaratibu huo ili changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita zisijirudie tena.



Udhibiti ubora wa mbolea



Juu ya udhibiti wa ubora wa mbolea alisema, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ilisajili jumla ya wafanyabiashara wa mbolea 533 na kuwapa leseni za kufanya biashara hiyo. Alisema jumla ya tani 36.7 za mbolea zilikuwa chini ya kiwango na hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya kampuni zilizokutwa na mbolea hizo.

Pia Waziri Chiza alisema kuanzia msimu wa 2013/2014 Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) ilikuwa na akiba ya nafaka tani 25,453 ambapo katika mwaka 2013/014 NFRA ilinunua tani 219,377 na kufanya jumla ya akiba ya nafaka kuwa jumla ya tani 244,830.



Wazalishaji wa sukari



Alisema kumekuwa na malalamiko ya wazalishaji wa sukari nchini juu ya kushindwa kuuza sukari katika soko la ndani kutokana na hisia kuwa kiasi kikubwa cha sukari kimeingizwa nchini bila kuidhinishwa na Serikali.

Alisema kutokana na hilo wizara na wadau wa sukari waliazimia kuundwa kwa kikosi kazi kitakachotafiti na kutoa mapendekezo ya mfumo mzuri wa kuagiza sukari.

Waziri Chiza alisema uzalishaji wa sukari katika viwanda vya Kilombero, Mtibwa, TPC na Kagera ambapo hadi Machi 31, mwaka huu ulikuwa tani 293,011 sawa na asilimia 99.9 ya malengo.



Mbegu za pamba



Alisema changamoto kubwa iliyojitokeza katika msimu wa 2013/2014 ni tani 1,088 za mbegu ya pamba isiyokuwa na manyoya inayotayarishwa na Kampuni ya Quton zilizosambazwa kwa wakulima kutokuota.



Alisema Wizara ilifanya tathmini ya mbegu yote iliyoharibika katika maeneo yaliyoathirika na wakulima walipewa mbegu mbadala.



“Wizara haitailipa Kampuni ya Quton Sh bilioni 1.7 ya ruzuku ya mbegu ambayo haikuota,” alisema.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Profesa Peter Msolla alisema dhana ya kilimo kwanza haijatoa matunda ambayo yalitarajiwa.



“Kamati imebaini pamoja na kuwepo kwa mikakati ya Kilimo Kwanza, utekelezaji wake hauko dhahiri Kamati inashauri Serikali ifanye tathmini juu ya mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa azma hii,” alisema.



Alisema pia Serikali itapima maeneo ili kupata matumizi bora ya ardhi kutokana na migogoro mingi inayohusu matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji , wakulima na wawekezaji, wananchi na mamlaka za hifadhi za Taifa.



“Serikali iweke juhudi za makusudi kupima maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi, Serikali isisite kuchukua hatua kwa wawekezaji waliochukua maeneo makubwa ya ardhi na hayaendelezwi mpaka sasa na kuwapa wananchi kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo na ufugaji, ”alisema.




No comments: