HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA DAR ES SALAAM,TAREHE 22 DESEMBA, 2014
Shukrani
Mheshimiwa Makamu wa Rais;
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi wa CCM Mkoa;
Viongozi Wenzangu;
Viongozi wa Dini;
Wazee Wangu;
Wananchi Wenzangu;
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi wa CCM Mkoa;
Viongozi Wenzangu;
Viongozi wa Dini;
Wazee Wangu;
Wananchi Wenzangu;
Nawashukuru
sana wazee wangu wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wangu na kuja
kuzungumza nami siku ya leo. Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya muda
mfupi lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki. Naomba radhi kwamba
ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu
tukaahirisha mpaka leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu.
Kama
mjuavyo, kila ninapoomba kukutana nanyi ninalo jambo au mambo muhimu
kitaifa ambayo napenda kuzungumza nanyi, na, kwa kupitia kwenu taifa
zima linapata habari. Leo nina mambo mawili.
Wazee Wangu;
Kwanza
kabisa, nataka kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu
wa upendo mliouonyesha kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba watu wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu kuendelea kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.
wa upendo mliouonyesha kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba watu wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu kuendelea kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Jambo
la kwanza ninalotaka kulizungumzia leo ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba, 2014 na jana tarehe
21 Desemba, 2014 katika maeneo ambayo uchaguzi huo uliahirishwa. Bila
ya shaka sote tumesikia taarifa ya awali ya zoezi la upigaji kura
iliyotolewa na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, TAMISEMI tarehe 17 Desemba, 2014. Katika taarifa yake hiyo,
Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi limeenda vizuri kwenye
maeneo mengi nchini. Uchaguzi ulifanyika kwa ukamilifu katika
Halmashauri 141 kati ya 162. Katika Halmashauri 21 uchaguzi wake uliahirishwa na umefanyika jana tarehe 21 Desemba, 2014.
Kwa
jumla, katika maeneo mengi uchaguzi ulifanyika kwa salama na amani na
hivyo kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda kuongoza
vijiji vyao, vitongoji vyao na mitaa yao. Kufanyika kwa uchaguzi huu ni
uthibitisho mwingine wa kuendelea kukomaa kwa demokrasia
nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa wale wote
walioshiriki katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama vya siasa na
wagombea. Natoa pongezi maalum kwa walioshinda. Nawaomba sasa wakae
chini kutengeneza mikakati na mipango ya kuwaongoza wananchi wa maeneo
yao katika kupata ufumbuzi wa changamoto za maendeleo na za maisha,
zinazowakabili.
Ndugu wananchi;
Katika
taarifa yake hiyo pia, Waziri Hawa Ghasia alielezea masikitiko yake
kuhusu kasoro za uendeshaji wa zoezi zilizojitokeza katika maeneo
mbalimbali. Aidha, aliahidi kuchukua hatua stahiki za kinidhamu dhidi
ya watendaji na viongozi wa Serikali waliosababisha kasoro
hizo. Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni
pamoja na kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi, kushushwa cheo, kukatwa
mshahara au kupewa onyo.
Napenda
kuelezea kufurahishwa kwangu na msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na
nampongeza kwa hatua alizochukua. Namuunga mkono na namtaka aendelee na
msimamo huo katika kukabili vitendo vya utovu wa nidhamu wa watumishi
wa umma. Lazima kila mtumishi wa umma ajue kuwa asipotimiza ipasavyo
majukumu yake kuna adhabu inayolingana na kosa alilofanya. Isitoshe,
watu hao ndio watakaoendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwakani
wakiwa mawakala na wasaidizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo basi,
kuwajibishwa wale waliozembea katika uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na
kwa wengine katika uchaguzi wa mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.
Ndugu wananchi;
Kwa
upande wa ghasia, fujo na ugomvi uliotokea wakati wa zoezi la uchaguzi,
nimezungumza na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na kuwataka
kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo vya kuvunja sheria
wanatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nimewataka
wasifanye ajizi na watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari ambao hawana
budi kuchukuliwa hatua thabiti za kuwadhibiti na kuwaadabisha.
Tusipofanya hivyo tunawakatisha tamaa raia wema na watiifu wa
sheria. Aidha, watu wakikamatwa na kuachiliwa muda mfupi baadae, wakati
mwingine hata bila dhamana ya namna yo yote inawachanganya sana watu
wema. Isitoshe tutakuwa tunalea maradhi ya watu wabaya na kuwafanya
waendelee kusumbua jamii. Nimewakumbusha kuwa wasipokuwa wakali
sasa tunaweka mazingira ya hatari ya kuja kutokea mambo mabaya
zaidi mwaka ujao kwenye uchaguzi mkuu.
Sakata la Akaunti ya Tegeta ESCROW
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kulizungumzia si geni masikioni kwenu, nalo ni
sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa
wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014, kulitolewa madai
kuwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki
Kuu zimechotwa kinyemela na mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power
Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa wa Serikali.
Serikali
iliahidi kufanya mambo mawili. Kwanza, kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa Akaunti hiyo na
kwamba taarifa yake itawasilishwa Bungeni. Na, pili, kumuagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
kufanya uchunguzi wa mwenendo mzima wa miamala katika Akaunti hiyo na
kama kuna uhalifu wo wote uliopo kwenye mamlaka yake achukue
hatua zipasazo kwa mujibu wa mamlaka na madaraka aliyonayo.
Ndugu Wananchi;
Yote
mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali amefanya ukaguzi wa miamala katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta
iliyoko Benki Kuu na taarifa yake ilishawasilishwa Bungeni. Pia
niliagiza taarifa hiyo ichapishwe kwenye magazeti na tovuti ya Serikali
ili watu waweze kuisoma. Agizo hilo nalo limetekelezwa.
TAKUKURU wameendelea na uchunguzi wao na watakapomaliza na kuridhika
kuhusu makosa yaliyofanywa watawafikisha wahusika
Mahakamani. Mkurugenzi Mkuu wa PCCB alifika kwenye Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala hili
aliyoyaona ni muhimu Kamati iyajue.
Mambo Manne Makuu
Ndugu Wananchi;
Tarehe
8 Desemba, 2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa
nilikabidhiwa taarifa mbalimbali kuhusu sakata hili. Tangu wakati huo
nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali na kuagiza
nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika. Shabaha
yangu ni kuyaelewa vizuri mambo hayo ili niweze kufanya uamuzi ulio
sahihi na wa uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu manne:-
(a) Akaunti ya ESCROW
(b) Miliki ya PAP kwa IPTL
(c) Kodi za Serikali, na
(d) Tuhuma za Rushwa
Akaunti ya ESCROW
Ndugu Wananchi;
Katika Mikataba ya Kununua Umeme (Power Purchase Agreements)
ambayo TANESCO imetiliana sahihi na kampuni binafsi za kuzalisha umeme
za IPTL, SONGAS, SYMBION POWER na AGGRECO, kuna malipo ya namna mbili
yanayofanywa na TANESCO. Kwanza, hulipia umeme ilionunua kutoka kwa
kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy charges). Na, pili hulipia gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo, yaani tozo ya uwekezaji (capacity charges).
Katika mikataba yote hiyo imekubaliwa kuwa iwapo kutatokea
kutofautiana, au mzozo unaohusu uwekezaji, upo utaratibu wa usuluhishi.
Utaratibu huo unataka kwanza kufanyike mazungumzo, wakishindwa kuelewana
watafute mtu wa kuwashauri na kuwasuluhisha; wakishindwa kukubaliana
wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama) cha Kimataifa cha Usuluhisi
wa Migogoro ya Uwekezaji, (International Centre for Settlement of
Investment Disputes – ICSID) kilichopo London, Uingereza.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
1998 TANESCO walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa
Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za
IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001 Kituo
cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya TANESCO
yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola za Marekani 127 na siyo Dola milioni 163.17 walizodai IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity charges) nayo ilipunguzwa kutoka Dola za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo.
Ndugu Wananchi;
Miaka
minne baadaye TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu
zaidi. Waliamua kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka
2001. Nimeambiwa kuwa wanasheria wa TANESCO walishauri Shirika hilo
lidai ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa IPTL ufanyike kwa
kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi 50,000 badala ya kutumia msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola za Marekani milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1.
Wakati
wakisubiri mchakato wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande zote
mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Tarehe 5
Julai, 2006, akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa sahihi na
IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO
upande mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala wa kutunza
akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.
Ndugu Wananchi;
Kwa
mujibu wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL iliendelea kupeleka madai ya
tozo ya uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika kulipa madai
hayo. Malipo hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya
Tegeta tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa
moja. Utaratibu huu mpya ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili
zitakapofikia mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji. Kwa upande wa
malipo ya gharama ya umeme (energy charges) TANESCO imeendelea kulipa moja kwa moja kwa IPTL bila kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na mgogoro.
Ndugu Wananchi;
Kwa
miaka saba tangu tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka
tarehe 5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi shughuli zote
za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi
wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na TANESCO. Pande mbili
husika hazikuwahi kukaa kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa
kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama
ilivyofanyika mwaka 1998.
Wakati
wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya IPTL
na kupeleka malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji ulisimama
katika kipindi kifupi wakati kampuni ya IPTL ilipowekwa kwenye
ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti hiyo inafungwa
tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi 8,020,522,330.37; Hatifungani zenye thamani ya shilingi 159,231,370,000 na Dola za Marekani 22,198,544. Fedha zote hizo ni sawa na shilingi bilioni 202.9.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo, wakati huo Akaunti hii ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati Akaunti inafungwa TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni 103.8. Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa riba ya asilimia mbili ya fedha zote ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo basi, riba iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za Marekani milioni 33.6.
Ni
matumaini yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu sawa na
sahihi kuhusu kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya ESCROW siku
uamuzi wa Mahakama ulipofanya akaunti hiyo ifungwe. Kwa kifupi Taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaeleza kuwa Akaunti
hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi bilioni 306.7 kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Fedha za Nani
Maelezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu fedha ni za nani!!!
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu pia kwamba maelezo haya kwa kiasi fulani yamesaidia
kutoa jibu kwa swali maarufu la fedha za kwenye akaunti hii ni za
nani? Je ni za umma au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea Akaunti ya
ESCROW ni nini? Akaunti ya ESCROW ni tofauti na akaunti nyingine
tunazozijua katika Benki zetu ambazo mtu anaweka fedha zake. Kama
tujuavyo, katika Benki zipo Akaunti za aina tatu ambazo wengi
tunazifahamu na kuzitumia yaani Akaunti ya Akiba (Savings Account),
Akaunti ya Hundi (Current Account) na Akaunti ya Muda Maalum (Fixed
Deposit Account). Akaunti ya Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa
ajili ya kufanya kazi maalum, kwa masharti maalum na kazi hiyo ikiisha
akaunti yenyewe hufungwa. Akaunti hiyo husimamiwa na wakala
aliyeteuliwa kwa makubaliano ya wale wanaofungua akaunti hiyo. Wakala
ndiye mwenye jukumu la kusimamia akaunti na kumlipa mwenye fedha wakati
ukifika. Kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta pande mbili husika
zilikubaliana kuwa Benki Kuu ndiyo iwe Wakala. Ni muhimu kujua kuwa
akaunti hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye Benki yoyote siyo lazima BoT.
Akaunti ya Tegeta ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges)
zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa
ambaye ni IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa
IPTL. Kama nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili kutoa nafasi
kwa pande hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango cha
tozo ya uwekezaji ya IPTL.
Kimsingi
basi, fedha hizi ni za IPTL kwani ndiye mlipwaji na ni malipo
yanatokana na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji. Hata
hivyo, kwa mujibu wa CAG, inawezekana katika fedha hizo kuna fedha za
umma. Hi ni kwa namna mbili.
Kwanza, kama
mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha tozo ya
uwekezaji kupungua kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika ICSID-1 na kama
pande mbili husika zingekubaliana au kuagizwa kuwa punguzo hilo lianze
kuhesabiwa tangu tarehe ilipofunguliwa Akaunti hiyo (tarehe 5 Julai,
2006), basi kungekuwepo pesa za kurejeshwa TANESCO. Maadamu hili
halikufanyika mpaka Mahakama ilipofanya uamuzi uliosababisha akaunti
hiyo kufungwa. Katika mazingira hayo fedha zote zinakuwa ni za IPTL
maana hakuna madai ya TANESCO.
Ndugu Wananchi;
Namna
ya pili ni ile ambapo katika fedha hizi kunaweza kuwepo fedha za umma
na iwapo kuna kodi za Serikali ambazo hazijalipwa. Kwa mujibu wa
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
kuthibitishwa na TRA ni kwamba kulikuwa na kodi ya VAT ambayo
haikulipwa. Nimeambiwa kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu wa kukata
kodi hizo kabla ya kulipa madai ya IPTL lakini kwa baadhi ya malipo
haikufanyika hivyo. Hivi IPTL inastahili kudaiwa kodi ya Serikali? Kwa
mujibu wa tathmini iliyofanywa, kodi inayotakiwa kulipwa na IPTL ni shilingi bilioni 21.7. IPTL wameshapelekewa madai na TRA, na IPTL wamekubali kulipa.
Katika
ukaguzi wa Hesabu za TANESCO za mwaka 2012, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali aliwaelekeza TANESCO kuacha kuhesabu fedha zilizopo
kwenye Akaunti ya ESCROW kama ni fedha zao. CAG aliwaambia TANESCO
kwamba fedha hizo si zao.
Maagizo hayo ya CAG yanasomeka kama ifuatavyo:
“As
a result, the deposit balance in Escrow account does not meet the
definition of an asset of the Company and therefore an adjustment has
been made to de-recognize the asset and related liability to the tune of
the amounts available in the Escrow account”
Kwa
tafsiri yake ni kuwa: “Hivyo basi, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya
Escrow hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni mali ya kampuni (TANESCO)
hivyo, marekebisho yamefanywa ili kutotambua mali na madeni yanayohusu
fedha hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow.”
Kutokana
na maelezo haya ni dhahiri kwamba, fedha zilizokuwa kwenye Escrow siyo
za TANESCO na hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu vya TANESCO kama mali
yake.
Chimbuko la Sakata
Wazee Wangu;
Chimbuko
la kadhia yote hii Bungeni na kwenye jamii ni uamuzi wa tarehe 5
Septemba, 2013, wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kuitambua PAP kuwa
mmiliki halali wa IPTL na kuagiza Mfilisi akabidhi shughuli zote za IPTL
kwa PAP. Katika utekelezaji wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu
ukazuka mjadala mkali kuhusu fedha zilizomo kwenye akaunti ya ESCROW
kukabidhiwa kwa PAP. Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya Serikali
miongoni mwa viongozi na watendaji wa Wizara na Taasisi zinazohusika
moja kwa moja na akaunti hiyo. Hizi ni Wizara ya Nishati na Madini,
TANESCO na Benki Kuu. Viongozi na Watendaji husika walikuwa wanajiuliza
na kuuliza kama walipe au wasilipe. Walipotaka ushauri wa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali wakaelekezwa watekeleze uamuzi wa Mahakama
Kuu. Alisema uko sawa na hauna matatizo. Halikadhalika, Benki Kuu
walipoulizia kuhusu kodi za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
alielekeza kuwa hakuna kodi ya kulipwa.
Kwa
kuzingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, malipo yakafanyika
kwa IPTL tena bila ya kodi kulipwa. Baada ya malipo kufanywa ndipo
mjadala huo ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka kuwa kadhia kubwa
iliyochukua sura ya kashfa yenye dalili za rushwa na wizi.
Uamuzi Unaotiliwa Shaka
Wazee Wangu na Ndugu Wananchi;
Kwa
jumla uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu akaunti ya Escrow, ushauri wa
Mwanasheria Mkuu kwa Serikali wa kuelekeza uamuzi huo utekelezwe na
viongozi wa Serikali kutekeleza ushauri huo vimetiliwa
shaka. Umeonekana kuwa haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara
nchi. Isitoshe uamuzi huo umeibua hisia za kuwepo harufu na vitendo vya
rushwa. Wapo waliosema si bure iko namna! Wapo waliotaja majina na
watu wanaodai wamepata mgao wa Escrow tena wengine wamechukua fedha kwa
viroba, sandarusi na rumbesa. Bahati mbaya sana katika mjadala
ilijengeka dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na
Maafisa hao wa Serikali kwa nia ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli ni
kwamba uamuzi ulifanywa na Mahakama Kuu na kwenye Serikali ilikuwa
utekelezaji wa amri hiyo.
Wazee Wangu;
Nilipokutana
na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata maoni yake kuhusu
kadhia hii ameendelea kusema alichosema Bungeni kuwa hakukosea katika
ushauri wake na wala Mahakama haikufanya makosa. Hivyo basi, hakuona
sababu ya kwenda Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi wa Mahakama
kuhusu fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta kukabidhiwa
kampuni ya PAP mmiliki wa IPTL. Vilevile haoni kama kuna hasara yo
yote ambayo nchi imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL na imelipwa
IPTL.
Akifafanua,
alisema kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa ajili ya kutunza fedha
za malipo ya tozo ya uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa yanafanywa na
TANESCO. Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo na kuanzishwa
kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ilikuwa inalipa tozo ya
uwekezaji moja kwa moja kwa IPTL. Baada ya kutokea mzozo na akaunti
kuanzishwa mambo mawili hayakubadilika. Kwanza kwamba IPTL haikuacha
kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO. Na, pili, kwamba
TANESCO haikuacha kulipa madai hayo. Mdai na mdaiwa
hawakubadilika. Kuwepo kwa akaunti ya Escrow hakubadili mwenye fedha
zake. Akaunti hiyo iliundwa kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu
inatafutwa kuhusu kiwango cha tozo. Matumaini ni kwamba kama kiwango
kitapunguzwa, TANESCO inaweza kupata nafuu ya malipo.
Kuhusu
uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe fedha za akaunti ya Escrow,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni uamuzi sahihi na wala taifa
halikupata hasara kwa sababu pesa zimelipwa IPTL na siyo mtu
mwingine. Isitoshe anaona uamuzi wa Mahakama umeisaidia TANESCO kutua
mzigo mkubwa iliyokuwa nao kwa miaka saba.
Kama
mjuavyo, akaunti ya Escrow ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya tozo
ya uwekezaji ya IPTL. Ilianzishwa kwa matumaini kuwa TANESCO watapata
nafuu ya tozo ya uwekezaji. Lakini, hapakuwahi kufanyika mazungumzo
baina ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo na wala suala hilo
halijafikishwa ICSID. Haikuweza kufanyika hivyo kwa sababu washauri wa
kisheria wa TANESCO hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai kuwa hawafanyi
hivyo kwa sababu hakuna sababu mpya zinazoweza kupatikana kuifanya ICSID
ibadili uamuzi wake wa 2001 kuhusu kiasi cha tozo na namna ya
ukokotoaji wake.
Matokeo
yake ni TANESCO kuwa na akaunti ya Escrow ambayo mwisho wake
haujulikani. TANESCO inaendelea kudaiwa na IPTL tozo ya uwekezaji na
kulazimika kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti ya akaunti ya
Escrow wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa mujibu wa taarifa ya
CAG mpaka tarehe 20 Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 103.8ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola za Marekani milioni 33. Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti ya Tegeta Escrow unalipatia unafuu TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni na riba.
Kwa
upande wa kodi za Serikali ambazo hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji Werema
alisema yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama mamlaka husika inaona
zipo kodi zinazostahili kulipwa izidai. Hakuna kilichopotea kwa sababu
anayedai, yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo, IPTL.
Uamuzi wa ICSID II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji
Wazee Wangu;
Yalitolewa
mawazo kuwa kama fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zingelipwa baada ya
uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji
(ICSID II) kutoa uamuzi wake, TANESCO ingepata nafuu ya kupungua kwa
tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba kuna mambo
mawili ya msingi. Kwanza kwamba Mahakama hiyo haikutoa viwango vipya
vya tozo kama ilivyofanya mwaka 2001 kwenye ICSID–I. Haikubadili
mwongozo wa ukokotoaji wa tozo. Imesema madai yanaweza kuzungumzwa na
kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo TANESCO watambue kwamba wanahisa
waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa kununua mtambo na pia walikopa
madeni, na kwamba kiasi cha fedha walichowekeza kilitakiwa kiwe na
kiwango cha juu zaidi cha faida.
Jambo
la pili ni kwamba, shauri hili la pili la ICSIDI II halikuihusisha
kampuni ya IPTL mwenye Mkataba wa Kuuza Umeme na TANESCO na siyo Benki
ya Standard Charterd. IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji wa uamuzi
wa shauri hilo hapa nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa TANESCO kufanya
mazungumzo kwa msingi wa shauri hilo.
Kinga Dhidi ya Madai
Wakati
wa kufunga akaunti ya Escrow, upande wa Serikali ulielezea hofu yake ya
uwezekano wa siku za usoni mtu kudai tena kulipwa fedha hizi hizi
ilizolipwa PAP. Nimeambiwa kuwa suala hilo haliwezi kutokea kwani
limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia. PAP imetiliana sahihi
na Serikali kwamba iwapo kutatokea mdai yo yote PAP itawajibika kulipa.
Mashaka ya Miliki ya PAP kwa IPTL
Ndugu Wananchi;
Hofu
nyingine kuhusu uwezekano wa Serikali kupata hasara ni yale madai kuwa
huenda miliki ya PAP kwa asilimia 70 za hisa za IPTL zilizokuwa za
kampuni ya Mechmar Berhard ya Malaysia siyo halali. Pale mwanzoni
ilidaiwa kuwa kampuni ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya Piper
Link ya British Virgin Islands ilikuwa chini ya mchakato wa ufilisi
kule Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria mtu hawezi kuuza hisa zake
akiwa kwenye mazingira hayo. Katika uchunguzi wa CAG alieleza kuwa
amethibitisha kwamba madai hayo si kweli, Mechmar walipouza hisa zao
tarehe 9 Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye ufilisi. Iliingia kwenye
mchakato wa ufilisi mwaka 2012.
Lakini
kwa upande wa kampuni ya Piper Link ya Uingereza inasemekana iliuza
hisa hizo baada ya kuwa wamepokea amri ya Mahakama ya Malkia ya BVI
kuizuia isiuze hisa hizo. Je ni kweli? Imefanyika hivyo? Kama ni
kweli je PAP waliponunua hisa hizo walijua kama kuna zuio au
hapana? Kama walijua basi na wao ni sehemu ya njama za kufanya
udanganyifu. Kama hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza
uchunguzi wa kina ufanyike kupata ukweli. Natambua hivi sasa Mahakamani
zipo kesi zinazohoji uhalali wa PAP kumiliki asilimia 70 za hisa za
Mechmar Berhad. Uchunguzi wetu hautaingilia mchakato huo lakini unaipa
Serikali fursa nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu suala hili lenye
mjadala mkubwa.
Jambo
lingine muhimu ambalo limeleta matatizo kwa Mahakama zetu nchini na
BRELA ni uuzaji wa hisa za IPTL au kuwekwa rehani hisa hizo bila ya
uamuzi huo kusajiliwa BRELA na kwenye Mahakama zetu. Sheria zetu
ambazo ndizo za nchi ya Jumuiya ya Madola kama ilivyo kwa Hong Kong,
Malaysia, na BVI, inaitaka kampuni ya Piper Link ya BVI iliponunua hisa
za Mechmar katika IPTL kusajili BRELA ununuzi huo. Hali kadhalika,
inaitaka SCB ya Hong Kong na kupata amri ya Mahakama kuzuia deni la
Mechmar na kuwekwa dhamana ya hisa za Mechmar katika IPTL. Piper Link
isiuze hisa 70 za Mechmar katika IPTL. Walitakiwa wasajili na BRELA na
Mahakama yetu. Kutokufanya hivyo ndiko kunazua maneno mengi na mzozo
kuhusu uuzaji wa hisa hizo kwa PAP. Kwa SCB wanapata usumbufu wa kudai
madeni yao IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi utakaofanyika utapata
ukweli wa yote kwa uhakika.
Ndugu Wananchi;
Taarifa
niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza nanyi ni kuwa katika Mahakama
zetu nchini kuna mashauri yahusuyo miliki ya PAP ya hisa 70 zilizokuwa
za Mechmar katika IPTL na yapo mashauri yahusuyo PAP kupewa fedha za
akaunti ya Escrow. Zipo pia nyingine za masuala mbalimbali yakiwemo
mashauri yaliyofunguliwa na PAP dhidi ya watu, na makampuni binafsi na
vyombo vya Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama zetu utatoa majibu kwa
masuala yote hayo.
Pamoja
na hayo yatakayokuwa yanaendelea Mahakamani, Serikali itaendelea
kufanya uchunguzi wake na kuamua namna ya kushughulikia taarifa
zitakazopatikana ili nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu kufanya
hivyo.
Jambo
lingine muhimu nataka uchunguzi wa kina ufanyike ni kujua nani ni nani
katika uuzaji na ununuzi wa hisa za Mechmar. Hususan nataka tujue kwa
ukweli na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa bei gani. Je, ni kweli gharama
zinazosemwa ndizo zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli huo ili tujue
kodi yetu ya ongezeko la mtaji (Capital Gains Tax) inayostahili kulipwa Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani kimelipwa na kipi hakijalipwa ili kidaiwe?
Tuhuma za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa
Wazee Wangu;
Kumekuwepo
na tuhuma za vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa kufunga
akaunti ya Escrow na kukabidhi fedha hizo kwa kampuni ya
PAP. Halikadhalika, kumekuwepo na hisia hizo hizo kwa upande wa jinsi
kampuni ya VIP Engineering and Marketing ilivyotumia pesa zake zilizoko
kwenye Benki ya Mkombozi. Yamesemwa mengi sana na mmeyasikia na
kuyasoma.
Rushwa
ni kosa la kijinai ambalo kwa Serikali yetu ni kosa ambalo ni vigumu
kulivumilia wala kulifumbia macho. Mara baada ya kupata fununu za
uwezekano wa vitendo hivyo kufuatia taarifa ya awali ya CAG ya kwenda
kukagua miamala, niliagiza taarifa husika zifikishwe kwenye Taasisi ya
Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa uchunguzi zaidi. Naambiwa taarifa
hizo zimefika na kazi ya uchunguzi inaendelea. Tayari watu kadhaa
wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa. Wakati nawasihi wananchi
kuvuta subira ili tuwape nafasi PCCB wakamilishe kwa ufanisi wa hali ya
juu kazi yao waliyokwishaianza, nawaomba PCCB waongeze kasi ya
uchunguzi. Napenda kufafanua kwamba kwa upande wa miamala iliyotoka
katika akaunti ya kampuni ya VIP Engineering and Marketing ya Ndugu
James Rugemalila, Serikali inashughulika na watumishi wa umma kwa
kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma, maana suala lao ni la
kimaadili. Hatuwahoji wasiokuwa watumishi wa umma.
Maazimio ya Bunge
Ndugu Viongozi;
Wazee Wangu;
Ndugu Wananchi;
Niliona
nianze kwa kutoa maelezo hayo ya utangulizi kabla ya kuyazungumzia
maazimio ya Bunge. Serikali imepokea maazimio hayo ya Bunge na
kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji wake. Nawapongeza Wabunge wetu
kwa moyo waliouonesha wa kuchukia maovu na kutaka yashughulikiwe
ipasavyo. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja nao. Nampongeza
Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu
Spika na Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu kwa uongozi wao
mahiri. Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini chini ya uongozi wao mambo
yameisha salama na tumepata maazimio nane yanayozungumzika na
kutekelezeka. Nawashukuru na kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Deo Filikunjombe na pia Wajumbe
waliounda Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia mwafaka wa mapendekezo haya 8
ambayo yaliazimiwa na Bunge.
Mwisho
lakini si ya mwisho kwa umuhimu, nawapongeza Wabunge wote kwa michango
yao mizuri. Jambo lililonifurahisha sana ni ushirikiano wa Wabunge wa
kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili muhimu,. Hivi ndivyo
inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze mshangao wangu
niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya maamuzi yale ni yao wao
na wenzao hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ina
Wajumbe19wa CCM na wa Upinzani 5. Bunge lina Wabunge wa CCM asilimia 74 na wa upinzani asilimia 26.
Hivi kama ni yao wao pekee na wa upande wa CCM wangepinga
yangekuwa? Yasingefika po pote, yangefia kwenye Kamati. Huku ni
kutafuta umaarufu kwa mgongo wa wengine. Na, Wabunge wengi wa CCM na
nyie semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote.
Napenda
kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu wa
dhamira ya kutekeleza yale maazimio yanayoangukia katika dhamana
yetu. Napenda kuainisha mtazamo na mwelekeo wa Serikali katika
utekelezaji wa maazimio hayo manane kama ifuatavyo:-
Azimio la kwanza: Serikali
iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Pendekezo
tumelipokea, ni jambo linalowezekana kufanya. Hata hivyo, tunapopima
ujumbe tunaoupeleka kwa jumuiya ya wawekezaji tunachelea kuwa inaweza
kuleta hofu na kuwatisha wawekezaji waliopo na wajao. Nalisema hivyo
kwa sababu sisi tuna historia ya kutaifisha mali za kamapuni
binafsi. Hofu hiyo bado ipo. Tukichukua mitambo hii tunaweza kurudisha
hofu za kurudi tulikokuwa na kukimbiza mitaji tunayohitaji kwa uchumi
kukua na nchi kupata maendeleo. Nashauri tuendelee kuyapatia ufumbuzi
matatizo ya IPTL kila tunapoyabaini. Aidha, Mahakama imetusaidia sana
kwa kuamuru mitambo ya IPTL ibadilishwe ili itumie gesi asilia na kutoza
bei ya umeme isiyozidi senti nane za Marekani. Tuyafuatiliye haya kwanza.
Azimio la Pili: Azimio
hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa Mikataba linasomeka
ifuatavyo: “Bunge limeazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la
Bunge mapema iwezekavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa
Bunge la Bajeti. Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio
ya mikataba ya umeme”.
Azimio
hili tumelipokea na tunaangalia namna bora ya kulitekeleza ili kuweza
kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kuitikia kilio cha muda mrefu
kuhusu uwazi katika mikataba ambayo Serikali inaingia na wawekezaji; na
pili kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki ya wawekezaji hao
dhidi ya washindani wao inazingatiwa. Serikali na Bunge tutakaa chini
hivi punde kutafuta namna bora ya kisheria na tutafanya hivyo kwa
kujifunza pia kutokana na uzoefu wa nchi ambazo zina utaratibu wa aina
hii.
Azimio la Tatu: Linasomeka;
“Bunge linaazimia kwamba TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine
husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahili kwa mujibu wa sheria
za nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye taarifa maalum ya Kamati
husika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya
ESCROW, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali
unaoendelea kuhusu kuhusika kwao katika vitendo hivyo vya jinai”
Vyombo
husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na
inaendelea. Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa mujibu
wa sheria.
Azimio la nne: Linasomeka,
“Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa zao wenyeviti wa Kamati za Bunge
waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP Engineering kabla ya kikao
kijacho cha Bunge”
Azimio hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe. Nawaachia wao waamue.
Azimio la Tano: Linasomeka;
“Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde
Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya Jaji
Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya
Tanzania”
Azimio
hili nimelipokea, tumelijadili hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa
kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa
suala kama hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa
Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais
aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inaporidhika
kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri suala hili
tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa.
Azimio la Sita: “Bunge
linaazimia kwamba mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja
Stanbic Bank Ltd. na benki yeyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa
mamlaka ya uchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa
katika akaunti ya ESCROW kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa
fedha haramu (Institutions of money laundering concerns).
Pendekezo
la Bunge ni zuri kwamba mamlaka husika na udhibiti wa vitendo vya
utakatishaji fedha vifanye uchunguzi kwa mujibu wa Sheria. Serikali
imelipokea na mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units
kulishughulikia. Naamini wameshaaza, tuwape muda watimize wajibu wao
kwa mujibu wa sheria.
Azimio la Saba: “Bunge
liliazimia kwamba Serikali iandae, na kuwasilisha Muswada wa
Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la kuanzishwa Taasisi
mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa
kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi,
kijamii na kisiasa.
Kazi
ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU inaendelea. Tayari Sheria
mbalimbali zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa ya mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Fedha
Haramu ya mwaka 1991 ambazo zote zinaweka utaratibu wa kushughulikia
vitendo vya rushwa. Tutaendelea kuziboresha sheria hizo kwa kadri
itakavyohitajika. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuimarisha usimamizi wa
sheria hizo. Jambo hilo nalo litazingatiwa katika maboresho hayo. Ni
dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza kupambana na kushinda vita
dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari kulifanyia kazi pendekezo lolote
linaloimarisha dhamira yetu hii njema.
Azimio la nane: “Bunge
linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi na
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi
wao.
Azimio
hili ndilo Azimio ambalo limevuta hisia za watu wengi, na pengine ndilo
ambalo utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji wake
umeanza. Kwanza, ni kuhusu Bodi ya TANESCO, tumeanza mchakato wa
kuunda Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza muda wake. Kuhusu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma
anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo
nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana
makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering and
Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule anayoimiliki na
kuiendesha. Mwenyewe ameeleza wazi kupitia vyombo vya habari. Pamoja na
hayo yapo mambo ya msingi kimaadili ambayo hayakuzingatiwa, hivyo
tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu Prof. Muhongo nimemuweka
kiporo, kuna uchunguzi niliagiza ufanywe na vyombo vyetu bado nasubiri
taarifa hiyo ili nifanye uamuzi ndani ya siku chache zijazo.
Hitimisho
No comments:
Post a Comment