Monday, January 12, 2015

MLEMAVU ALITUMIA MDOMO KUANDIKA MTIHANI WA SHULE YA MSINGI NA AKANG’ARA

MSICHANA mlemavu, Christine Kavandi Kavale, mwenye umri wa  miaka 17 kutoka kijiji cha Kutha, eneobunge la Kitui Magharibi mwa Kenya alitumia mdomo kuandika majibu ya KCPE na akatia fora baada ya kujizolea alama 317 kati ya 500 na kuibuka wa kwanza katika kitongoji. Licha ya msichana huyo kuwa na ulemavu wa miguu pamoja na mikono, alikuwa mwanafunzi taa katika Shule ya Msingi ya Kithyoko, wilayani Masinga huko Kenya.
Kulingana na Naibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bwana Boniface Masaka aliyemfunza Christine tangu ajiunge na shule hiyo, palikuwepo matumaini chungu nzima kwamba angefanya vyema kwenye mtihani huo wa kitaifa licha ya kukumbana na changamoto kedekede.

"Tumekaa naye tangu akiwa darasa la kwanza. Kwa vile mikono yake ilikuwa hafifu na haingeweza kushika vitu ipasavyo, tulimfunza  jinsi ya kutumia ‘mdomo wake kama mkono’ kushika kalamu ili aweze kuandika. Tuna furaha kwamba ameweza kufua dafu," Masaka ambaye pia anasimamia kitengo cha wanafunzi walemavu shuleni humo alielezea.
Mwalimu huyo alisema kuwa ilimbidi aliandikie shirika la mitihani ya kitaifa humo nchini (Knec) ili Christine aruhusiwe kutumia mdomo kuandika majibu ya mtihani wake kwenye makaratasi ya kawaida.
"Hangeweza kupigia mstari majibu yake kwenye vijikaratasi vya majibu (answer sheets) kama wale wanafunzi wengine," mwalimu alidokeza.
Wakati wa mahojiano hayo, Christine alikuwa amekaa kwenye kiti chake cha magurudumu huku mara moja mbili akionyesha ufasaha wake wa kuongea lugha za Kiswahili na Kiingereza.
Alihusisha matokeo yake na ‘bidii pamoja na kuwaheshimu wengine’.
"Nilitia bidii masomoni, nilikuwa napata ushauri kutoka kwa walimu wangu na vilevile niliwaheshimu wote niliojihusisha nao kwa njia moja ama nyingine," alieleza huku machozi ya furaha yakitiririka.
Msichana huyo hakusita kuelezea ndoto yake, huku akisema angetaka kujiunga na Shule ya Kitaifa ya Wasichana ya Alliance.
Alisema angependa kusomea Sheria.
"Ndoto yangu ni niweze kujiunga na Shule ya Alliance," Christine alisema.

Baada ya kupokelewa kwa matokeo yaliyotangazwa na Waziri Jacob Kaimenyi mwishoni mwa Desemba 2014 wanakijji, jamaa na wageni walimiminika nyumbani kwao kumpongeza.
Mfano wa kuigwa
Mamake, Bi Winfred Kavale aliarifu jinsi Christine ambaye ni kitinda mimba katika familia ya watoto wanne amekuwa mfano wa kuigwa kwani hakuruhusu hali yake ya maumbile ilemaze ndoto yake ya elimu.
Christine alisema somo lilokuwa mawe kwake ni Hesabu kwani hangeweza kuyakabili maswali yaliyohitaji kuchora au kupima akitumia vifaa vya kijiometri. Hata hivyo aliweza kunyakua alama 57 kwenye somo hilo.
Somo alilofanya vyema zaidi ni la Kiswahili ambapo alijizolea alama 71.
Wakati huo huo mbunge mteule wa chama cha Wiper kwenye Bunge la kitaifa Askofu Robert Mutemi ameitaka Knec kuwa ikitayarisha mitihani ambayo yaweza kufanywa na wanafunzi walemavu bila matatizo yoyote.
Mbunge huyu pia alimtaka mwezake wa Kitui Magharibi na ambaye pia ni kinara wa walio wachache Bungeni Bw Francis Nyenze amsaidie msichana huyu kwa kumpa ufadhili wa karo kupitia fedha za CDF huku akiitataka serikali kuwapa wanafunzi walemavu udhamini wa elimu.
Mwalimu Masaka alielezea matumaini yake kuwa Christine anaweza kufanya vyema zaidi kwenye shule ya sekondari ikiwa atapata vifaa vya kisasa vya kiteknolojia kumsaidia kwenye masomo yake.
"Naomba serikali kufanya juhudi kuhakikisha mwanafunzi huyu atakuwa na mazingara ya kufana kwa kuhakikisha atakuwa na vifaa kama kompyuta na head pointers vya kumsaidia kunakili kazi yake kwa urahisi bila kulazimika kutumia mdomo," mwalimu alisema.
Japokuwa Christine hajafikisha alama za kumwezesha kusajiliwa kwenye shule ya kitaifa yeye ana matumaini tele kuwa ndoto yake ya kujiunga na shule ya kitaifa ya Alliance Girls itatimia mwaka huu wa 2015

Source. swahilihub.com

13 comments:

Rahito said...

mungu amjalie afike mbali na watanzania tujitolee kuwasaidia watu kama hawa

SammyInfodaily Updates said...

daaaah its so fantastic megic i like hat
#dit

Unknown said...

Everything is possible when you believe and Trust Almighty God who can help you to overcome the Difficulties and challenges that may come on your way as well as Praying Also.
AMEN
#DIT

Unknown said...

mungu ameonyesha uwezo wa huyu binti atafika mbali#dit
by SEIF RAMADHANI

Fashion said...

mungu amsaidie aweze kufikia malengo yake
azidi kumpigania DIT

MKUDE said...

ACHENI MUNGU AITWE MUNGU #DIT
MKUDE PRISCA J

Unknown said...

Mungu akupi vyote wala hakunyimi vyote na pia usimzalau mtu mwenye ulemavu wa viungo vya mwili kwani anaweza kufanya vitu ambavyo uwezi kuzania.MHOKA Erick A. DIT/D/2014/0038

Unknown said...

MUNGU HUONESHA UTUKUFU WAKE KUPITIA WATU KAMA HAWA NAAMINI MUNGU ATAMSAIDIA NA ATAFIKA MBALI AMINA#DIT2014/2015 MWATOVOLWA CHARLES.

Unknown said...

Yatupasa tuliopewa Viungo kamili kizidisha Shukran Zetu Kwa Mola Mlezi wa Viumbe Vyote,,Na Kwa Mwenyezi Mungu hayo ni Mepesi Mno://DIT

Unknown said...

Viumbe wote wa mungu yatupasa kuamini kwa dhati kua"YOTE YANAWEZEKANA KWA MKONO WA MUNGU"
AMIN
MBIJE AMBELE .E.(DIT)

Unknown said...

wow,thats God's miracles.#AQU/D/12/T/0017

Unknown said...

so good
ANS/E/11/T/OO70

Rashid Mgohele said...

ashukuriwe MUNGU kwa kila jambo maana kazi yake haina kosa.
AGC/D/12/T/0050