Mwaka mpya umeanza na mambo mapya. Anghalab hii ni kauli ambayo umeisema baada ya mwaka huu kuanza. Kabla hatujaangalia kwa undani kauli hii, naomba nichukue nafasi hii kukutakia wewe msomaji wa TRACING CHALLENGES AND OPPORTUNITIES heri ya mwaka mpya 2015.
Ni jambo la kushukuru kupata nafasi ya kuuona mwaka huu na hivyo ni muhimu ukaitumia fursa hiyo vizuri ili uweze kuleta mabadiliko kwenye maisha yako.
Kila mwanzo wa mwaka, watu wengi huweka malengo mazuri kwenye maisha yao. Karibu kila mtu anasema nitaacha hiki, nitaanza hiki na kila mmoja anakuwa na matumaini makubwa kwamba kwa mwaka huo mpya, mambo yatabadilika. Ni siku chache baadaye, watu wanajikuta wanarudi kwenye maisha yao ya awali, wanaendelea kufanya yale ambayo wamekuwa wakifanya kila siku na hivyo maisha yao yanarudi kama awali.
Ukweli ni kwamba maisha yako hayawezi kubadilika kama wewe mwenyewe hutabadilika. Si ndugu, mwajiri, mteja au hata Serikali itakayobadili maisha yako. Wewe mwenyewe ndiyo unaweza kubadili maisha yako, na hupaswi kuleta mabadiliko hayo kwa maneno, bali kwa vitendo.
Leo tutapata nafasi ya kujadili misingi mitatu muhimu ya wewe kujijengea kwa mwaka huu 2015 na miaka yote ijayo ili kuweza kubadili maisha yako, kuyaboresha na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kwa kushindwa kujenga misingi hii kunaweza kuwa chanzo kikubwa cha wewe kuishi maisha ambayo huyafurahii.
KAZI
Msingi wa kwanza ni kazi. Kazi ndiyo msingi wa maendeleo kwa mtu yeyote na hata taifa lolote lile duniani. Ili watu waweze kuendelea, ni muhimu sana kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa. Moja ya kauli ninayopenda kuisikia ile isemayo kwamba hakuna kitu cha bure.
Ingawa watu wanafahamu kwamba kazi ndiyo msingi wa maendeleo, hapa kwetu Tanzania mambo ni tofauti kidogo. Watu wengi wanatafuta njia rahisi ya kufanikiwa kwenye maisha yao. Watu wanafikiria kupata kitu bila ya kutoa kitu! Ni katika hali hii ambayo tumekuwa na jamii ya watu ambao wanachukulia rushwa kama utaratibu wa kawaida katika maisha yao ya kila siku. Tumekuwa na jamii ya watu ambao wanakwepa majukumu yao, na badala yake wamebakia kulaumu tu watu wengine, taasisi na hata viongozi wao kwamba ndio kikwazo cha kutokufanikiwa kwao.
Hutaweza kufanikiwa kwenye maisha kama hupendi kufanya kazi, na siyo tu kufanya kazi, bali kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa. Ni lazima uwe tayari kuumia ili uweze kupata kile unachokitaka. Hakuna njia ya mkato hapo! Siku hizi kuna kamari iliyohalalishwa ambapo watu wanabashiri matokeo ya michezo na kama wakipatia wanapata fedha. Kamari hii kwa lugha ya Kiingereza, inaitwa betting. Kwa sasa inashika kasi kweli ndani ya nchi hii.
Ndugu yangu; hii siyo kazi na huwezi kufanikiwa kwa kushinda kamari au kushinda bahati na sibu. Hii ni michezo ambayo inakuondoa wewe kwenye lengo la msingi kwenye maisha yako. Fanya kazi ambayo inazalisha kitu, bidhaa au huduma ambayo inaweza kuboresha maisha ya watu wengine.
Chagua kazi ambayo upo tayari kuifanya, na unapenda kweli kuifanya, na ukishaianza, ifanye kwa moyo wako wote. Weka juhudi zako zote na weka ubunifu wako wote. Kufanya hivyo, kutakuweka katika nafasi nzuri ya kufanikiwa, bila ya kujali ni kazi gani unayofanya.
Hata hivyo, kama unaendelea kufikiri kuna njia rahisi ya kupata mafanikio bila kufanya kazi, au unakimbia majukumu yako au unafanya kazi kwa kusukumwa, naomba nikupe pole kwamba mwaka 2015 unakwenda kupotea huku ukishuhudia mwenyewe.
UAMINIFU.
Uaminifu ni msingi wako wa pili. Katika jambo lolote ambalo unafanya kwenye maisha yako, uaminifu ni muhimu sana.
Hivi sasa tunaishi kwenye dunia ambayo mafanikio yako yanategemea sana ushirikiano kutoka kwa watu wengine. Kama umeajiriwa mahali, unahitaji kuaminika kwa aliyekuajiri na pia kuaminika na wale unaofanya nao kazi!
Kama unafanya biashara, unahitaji kuaminika kwa wateja wako na pia unahitaji kuaminika kwa wale unaoshirikiana nao kwenye biashara. Jambo lolote ambalo ukilifanya litapunguza uaminifu wako kwa wale ambao wanakuzunguka, litakufanya ushindwe kufikia mafanikio unayotarajia.
Kwa vyovyote vile, hakikisha mwaka huu wa 2015 unakuwa mwaka ambao kwako unajijengea uaminifu kwa wale ambao wanakuzunguka. Tekeleza kile ambacho umeahidi! Kama umemwahidi mteja kwamba bidhaa au huduma unayomuuzia itakuwa na msaada kwake, hakikisha kwamba hilo linatimia. Kinyume na hapo, utaua biashara yako mwenyewe.
Kama umemwahidi mwajiri wako au mfanyakazi wako kwamba utakwenda kutekeleza jukumu fulani, hakikisha unafanya hivyo. Kama kuna kitu huwezi kufanya, kuwa muwazi, sema huwezi. Usikubali watu wategemee kitu kutoka kwako halafu wakikose na waishie kukuona wewe si mtu wa kuaminika.
Uaminifu ni msingi muhimu sana wa kujijengea kwa kuwa utakufanya uzungukwe na watu ambao wako tayari kukusaidia wewe kufikia malengo yako.
UADILIFU
Msingi wa tatu wa mafanikio ni Uadilifu. Ni muhimu wewe kuwa na vitu ambavyo unavisimamia katika maisha yako. Kumbuka kama huwezi kusimama kwa chochote, basi utaanguka kwa chochote. Lazima uwe na misingi yako, lazima uwe na mipaka ambayo huwezi kuvuka, na lazima uwe na viwango vyako vya kufanyia kazi.
Vitu vyote hivi ni lazima viendane na sheria na pia viwe vinawasaidia wengine. Kama hujajiwekea misingi ya kusimamia haki, ni rahisi sana kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa au ufisadi. Uadilifu ni muhimu sana kwako ili uweze kufikia mafanikio yoyote. Uadilifu utakufanya uweze kufanya kile ambacho ni sahihi bila ya kujali wengine wanakubali au la!
Uadilifu ni kuweza kusimamia haki yako na ya wengine bila ya kujali wengine wanafanya nini. Kwa hakika kabisa, ukosefu wa uadilifu umewafanya watu wengi kujikuta kwenye matatizo makubwa mno. Kuna watu unaweza kuona wamefanikiwa kutokana na wizi au ufisadi, lakini angalia maisha yao ya kila siku yakoje. Ni maisha ya wasiwasi, ambayo hayana furaha moyoni. Ni maisha yaliyojaa shaka wakati wowote.
Unapokuwa mwadilifu kwa kidogo unachopata, utaweza kukikuza zaidi na hatimaye kufikia mafanikio uliyokuwa ukiyatazamia.
Hii ndiyo misingi mitatu muhimu ya kujijengea kwa mwaka 2015. Fanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa. Kumbuka, hakuna kitu cha bure. Huwezi kupata kitu cha maana kwako bila kutoa jasho wala kuumiza akili.
Kuwa mwaminifu, kwa kutekeleza lile unaloahidi, na zaidi kuwa mwadilifu. Tenda lile ambalo ni sahihi, hata kama hakuna anayekubaliana na wewe. Jambo muhimu sana la kukumbuka, ni kwamba kitu chochote kizuri kwenye maisha, huwa hakiji haraka, hivyo unaweza kufanya mambo hayo matatu na bado siku zikaenda bila ya kuona mabadiliko. Nakuomba usikate tamaa, endelea kusimamia misingi hiyo mitatu na siku moja utaona matunda yake.
Nihitimishe kwa kukutakia kila la kheri kwa mwaka huu wa 2015, ukawe mwaka wa mabadiliko ya kweli kwako na yote unayotaka yaweke kwenye vitendo, huku ukitambua kwamba maneno matupu hayatakufikisha popote.
9 comments:
kujitambua na uadilifu ni moja kati ya njia za kupata mafanikio katka maisha so tujitambue na kufanya kaz kwa bidii kwa mafanikio yetu na ya taifa yetu
ts mi YUSUPH JUMANNE MSUTA
Kwanza tupende fursa zipatikanazo na kuzitilia mkazo wa utendaji, naamini tutafanikiwa. #Frank Matandura# DIT
daaah ni kweli kabisa...hasa uadilifu
SENDARO HALIMA SUPHIAN /DIT
kwa kweli...uaminifu, uadilifu ni vitu muhimu sana ili kufanikiwa.
KYAMLE LUCY N. /DIT
we real need to be punctual and flexible.Life is a life so fight for it.
It's good thing for all people's who want development in one way or another
Hey, a future is prepared today,so let do it now and not tomorrow,we have to work hard today in order to enjoy tomorrow,life is easy if you decide to do something for a positive benefits
Mbije ambele(dit)
Kuziona fursa ni kitu cha msingi sana, na pia kuzifanyia kazi. Asante kwa information.
MHAKO, Adam (FST/D/12/T/0022) FDS
Post a Comment