Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia bunge maalum la katiba bungeni Dodoma March 21, 2014 |
HOTUBA YA RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI
WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib
Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Pongezi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria
kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu
wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa
utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa
mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge
hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha
cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao
ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili
liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya
aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo yote na
watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu
yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa
kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora
wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja,
upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti
zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia,
rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha
amani, usalama na utulivu nchini. Katiba itakayostawisha zaidi
demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti
maovu. Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka
mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na
maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii
itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili
26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya. Mara ya
kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka
1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili
zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na
ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni.
Wananchi pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya
kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili
wapo wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa
Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata
hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio
waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge,
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii,
wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na
Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni
itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura.
Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu
kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko
hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi,
kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Kwa
ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
- Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama
ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki mwaka 1977.
- Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo
kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
- Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao
haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of
Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama
ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
- Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa
uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake
katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote.
Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge lilipewa
mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na
imani.
- Mabadiliko
ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia
Mgombea Mwenza.
- Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua
wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika
kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila
ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo na
Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya
kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha
Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya
badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi
vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti kwamba,
itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato wa
Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya
changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa
uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu
wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31
Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba
mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na
ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini,
siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika
pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe
16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa
kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza
maoni ya wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na
kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya
Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba
mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura
ya maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe
6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012
na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na
kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba,
2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba
kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014,
kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi
inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya.
Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho
kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu
ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine
yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya
Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma.
Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya
Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi
wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni
jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi
kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki na
kutoa maoni yao kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu,
wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao
muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja
na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini
na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi.
Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka
kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi,
kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi
ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge
hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa
Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa
wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa
Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la Tanzania.
Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa
mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi
yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa, imejumuisha dhana na
mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri
kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba
tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa
kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na
ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri
kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika
kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa
ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno. Hamna budi
kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa
dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile
ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa
msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya
hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha,
tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha
madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa.
Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi
yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la
kuepusha hali hiyo isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja
kitaonekana katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa
mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo
mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi
yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu
uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna
baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno
kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo
kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria
zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako
mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu
hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable).
Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima
yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba
tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo
pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo
kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari
na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu
inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa
“Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika
likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu
yake ya bahari”.
Maelezo
hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na
mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi
nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na
sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni
yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe.
Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni
mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa na muundo wa Serikali tatu
na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za
nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo ya taifa yameainishwa na
Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na
itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na
Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo,
ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na
kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya
Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya
Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru
wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa
Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano
majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati ya
Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu,
inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili
kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi
washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama
mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka
na Serikali ya Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu
Utumishi katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi
katika Rasimu. Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua
mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili
utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba
mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu
kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie
kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu
changa.
Mambo
ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo
la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge
kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita
mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”. Watu
hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na
hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande
kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na
kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe
vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi
hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko.
Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa
Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita
mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua
kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika
mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977
tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa
na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli anachostahili
Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili aendelee kutumikia
watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu kishawishi cha
kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema jambo hili
mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge.
Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!.
Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri
mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa
Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu
wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo
Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika
kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu
huo hapa kwetu. Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu
wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za
uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo
jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu
bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa.
Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa
wazi katika mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha
vuguvugu la kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza
kufanya kazi ya kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima
faida na hasa thamani inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba
tujiridhishe kama jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka
mitano kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu watu
wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya
mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu
lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili.
Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa
kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu linapendekeza
kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo
agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu
utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili.
Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi
usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu
tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania
inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara
kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya.
Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964.
Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka
1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka
1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga
ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi
wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali
mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo
unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha
Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya
Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua
kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu.
Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na
Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na
kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje
leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata
kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika?
Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki
katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa
marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa
Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko
hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you
must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu
ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania
Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia
60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia
61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na
endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa
na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu
hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo
wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume
imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu,
hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo
msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa
taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa
Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi
47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa
Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na
asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana
hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya
Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema
pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67),
inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano,
ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo
waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali
mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia
7.7 walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu
za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211.
Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa
Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine.
Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo
linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa
maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza.
Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa
maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote.
Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa
muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo
wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa Serikali
mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara
kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya
Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo.
Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya
Muungano, na kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka.
Wazanzibari pia, wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi
ya kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar
kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Aidha, kuna
malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11
mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa
mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa Muungano wa
Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya
watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano. Wanasema
Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa na
Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama
nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na
Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika
Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya
kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo
Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji
wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo baadhi
ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo
wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya
vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha Washirika wa
Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na hivyo,
utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia unawezesha kila
upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa.
Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo
kusaidia kukuza maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja
na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa muundo
wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa
na mchango muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu.
Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza gharama za
uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri
katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano.
Umezuia mkubwa kummeza mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha
hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964).
Aidha, umesaidia kudumisha amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja
na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto za
Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto zake.
Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama kubwa za
uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa
hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti.
Alisema kwamba: “watu …wanaodhani kuwa gharama
ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (Waulizeni Wazanzibari)
na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila
gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu kwamba
katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume
imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa gharama
za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika. Vilevile, kuna
uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya msingi
ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi
washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu
kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila
upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume
pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic
feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano.
Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in
decision making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa.
Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali
pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna
maana ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue
Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali
mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto zilizoainishwa na Tume
yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza matatizo ya
Muungano wetu bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo
kwa changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini
zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali
ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia
changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio
yaliyopatikana.
Katika
kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya Shelukindo
mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi
yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa
na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye Tume ya
Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31.
Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati ya
Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo
yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza.
Mambo hayo ni:
1. Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
2. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5. Usajili wa vyombo vya moto.
6. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali
zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa mabadiliko ya
Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
- Utafutaji
na uchimbaji mafuta na gesi asili.
- Ushirikiano
wa Zanzibar na taasisi za nje.
- Tume
ya Pamoja ya Fedha.
Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali kadhalika,
katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni nafasi
nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya Zanzibar na
ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile tunayo
dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa tofauti
zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu
orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali,
napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza
yale yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha
hiyo si hila za Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa
mambo yake ya ndani. Na, wala siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika
kutetea maslahi ya nchi yao. La hasha.
Pili,
naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano
kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote
mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa
kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja
ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa
kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano.
Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa
kila mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua
ukweli na undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na
kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
- Katiba
ya Jamhuri ya Muungano,
- Mambo
ya Nje,
- Ulinzi,
- Polisi,
- Hali
ya Hatari,
- Uraia,
- Uhamiaji,
- Biashara
ya nje na mikopo,
- Utumishi
katika Serikali ya Muungano,
- Kodi
ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
- Bandari,
Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati
ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi
kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na
kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za
Muungano zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za
kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe
maelezo kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
- Jambo
la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na
fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia
kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency
Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya
ililazimika kuwa na sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya
kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala
hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge
uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu
Urais tarehe 10 Juni, 1965.
Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
a. Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
b. Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
c. Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri wa Majini na kadhalika.
3.
Tarehe
22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali
ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa
ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya
Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
4.
Tarehe
22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16.
Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki
mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa
mwaka 1973.
5.
Mwaka
1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya
Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika
Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo
hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17,
Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu
kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
6.
Tarehe
17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na
kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama
Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea
nini kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na
sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye
yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi
yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila
yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika
Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa Serikali ya
Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi. Yale
yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa katika Orodha ya
Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande kushughulikia
ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na uamuzi
wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta
na gesi asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni
msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya baadhi ya mambo
katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya hivyo. Lililo
muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo maana,
mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za biashara, utafiti
na mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa
miaka kadhaa sasa na imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio
yetu kutumia fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na gesi asilia
lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu wakati wa
Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein msimamo
haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za
kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha Bungeni Muswada wa
Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo
yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza kukosa
majibu.
Hatimaye
wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga ya
“subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali
tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa
rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku
hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi.
Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala
la kiuchumi ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki,
mwani na kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na
kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki
rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana
tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na mashirika
ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi za nje bila kizuizi.
Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni ukweli
usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga hisia hasi
kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua
hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali. Hata zile kauli
kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka
itoke ionekane ili iache kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na
mazingira haya iliyonayo Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo
haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa
Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato
huu kuyamaliza mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara
ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana,
itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya
au taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka
yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu
mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar bila ya kulazimika
kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu yake.
Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza
wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba ya kuwabana
watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya
Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa
mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja
ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya
kisheria na kama hapana budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo
tutafanikiwa kuyaweka mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya
tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika
mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu,
wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto za Serikali
tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya kuzitatua. Tena yapo maoni ya
watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali tatu.
Nawaomba myatafakari kwa uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu ya
kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya
Muungano inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake
yenyewe za kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa
sababu hiyo inaweza kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo
itakosa ihsani ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni
mmoja wa washirika amefanya hivyo.
Pili,
kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha
kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa
unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika
wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake
chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya
Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi
washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati
mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato
yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi
washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika
mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa
kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni
rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama chanzo cha
kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa sababu ya kukosa
rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo kukopesheka. Kwa
jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu
wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye
yote wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga
maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa
hawana lo lote la kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa
Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu
hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu
unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu
kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na
inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa
hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi
yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza
kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia
inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi washirika. Bila ya shaka Bunge hili
likiamua tufuate mfumo huo linaweza kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo.
Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa
ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe
muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo
(deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo
muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic
sentiments) wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa
makini sana mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu
ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona
hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi.
Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni
lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani
yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama. Kama
hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana
kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua
kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani
Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu
fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na
raia wa nchi moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao
kuwa ni kati ya Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia.
Kwa mujibu wa sensa iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania
waliopo sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni Tanzania.
Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika,
watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalum wa
kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili.
Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi
rahisi tena kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara
moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi
kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi
cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku
wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto
hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za kweli.
Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya
Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye
hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda
yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote
mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye
itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa
ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na
wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na Muungano wetu unaweza
kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi
viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna budi
kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio sahihi.
Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na
mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano kusambaratika
halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa
kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi
waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono
yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu
tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta
tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi
kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle
ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku
moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo
yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila mtu
atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri
msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka
kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa
nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo
ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza
kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na
kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni
kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la
kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na
itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi
yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya
kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kuisoma
Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda wa
kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze kufanya uamuzi
ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na Watanzania
wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika
sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu.
Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache,
mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya
kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa.
Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba.
Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote.
Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa
nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi nzuri
iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la
Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake
haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza
kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu sote.
Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo
kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu
Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda
pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali hivyo
hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii
inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao
kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa
kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala
wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya wananchi wamekwazika sana na
mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo
waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya
baadhi yenu.
Ni
matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena katika
awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na
Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa nchi
yao. Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au
kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika
kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile
au hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa kutoka kwenu.
Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi
langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali maslahi
mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi yenu binafsi au ya makundi
yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania Kwanza”. Najua
kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo kwa kila jambo
litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi yao.
Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama misimamo hiyo
na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata
hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha mawazo
yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi wa pamoja
ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza mawazo ya
wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho
chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni watu
usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza kuwepo
kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba
muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya hivyo
hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi maarifa
wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya
kushirikiana na kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute kushindana,
hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima
Watanzania wote washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza
viongozi wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa kutambua na kuthamini
umuhimu wa kuwa na taratibu za mawasiliano, mashauriano na ushirikiano.
Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya
awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya hayo, tafadhalini zitumieni.
Jengeni madaraja imara zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba
nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa dini
tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende
salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi ulio
sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila watakaloliamua.
Baada
ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti
kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba.
Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya
Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment